under construction

Hotuba ya Bajeti kwa wizara ya ulinzi na JKT
E-mail Print PDF

HOTUBA YA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA, MHESHIMIWA SHAMSI VUAI NAHODHA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/2013.

UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, baada ya Bunge lako Tukufu kupokea taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013.

2. Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kuwasilisha hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka 2012/2013. Pili namshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Nawathibitishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote wa Tanzania kwamba nitatekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa

3. Mheshimiwa Spika, tatu napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri walioteuliwa kushika nyadhifa hizi hivi karibuni. Vile vile nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb.) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge. Nampongeza pia Mhe. Mussa Azan Zungu (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Vile vile napenda kuwapongeza Watanzania waliochaguliwa na Bunge letu Tukufu kuwa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

4. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2011/2012 Wabunge wenzetu watatu waliiaga dunia. Wabunge hao ni Marehemu Jeremia Sumari, Marehemu Mussa Silima na Marehemu Regia Mtema. Napenda kutoa pole za dhati kwako Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, ndugu, marafiki na Watanzania wote kwa ujumla kwa msiba huo mkubwa uliotupata. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao Peponi. Amin.

5. Mheshimiwa Spika, halikadhalika, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli kwa kutupa ushauri na mapendekezo mazuri sana wakati wakichambua mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu. Kamati hii imekuwa ikiishauri vyema Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu njia mbalimbali za kuimarisha utendaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa ili liweze kutekeleza majukumu yake ya Ulinzi wa nchi yetu.

6. Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maelezo yangu kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2012/2013 napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge kuwapongeza Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda (Mb), Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mhe. Dk. William Mgimwa (Mb), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Mheshimiwa Steven Wasira (Mb) kwa hotuba zao ambazo zimetoa mwelekeo katika masuala ya Mipango, Uchumi, Mapato na matumizi ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.

DIRA, DHIMA NA SHABAHA YA WIZARA

7. Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwa Taasisi iliyotukuka katika kudumisha amani na usalama wa Taifa. Aidha, Dhima ya Wizara hii ni kulinda eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya adui wa aina yoyote kutoka nje au ndani ya nchi na kuhakikisha uhuru na maslahi ya taifa vinalindwa. Kutokana na Dira na Dhima hiyo, shabaha ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kujenga na kuendeleza Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Vyombo vyake yaani Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na mashirika yake ya Mzinga, Nyumbu na SUMAJKT ili kuwa vya kisasa na imara katika kutekeleza majukumu yake.

MAJUKUMU YA WIZARA

8. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekabidhiwa majukumu ya kulinda uhuru na mipaka ya nchi yetu. Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966, majukumu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni saba. Kwanza, Wizara ina jukumu la kulinda mipaka ya nchi yetu. Pili, Wizara inasaidiana na Mamlaka za Kiraia katika kukabiliana na majanga ili kuwapatia wananchi waliofikwa na majanga misaada ya kibinadamu. Tatu, Wizara inashiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi zenye migogoro duniani. Nne, Wizara inaandaa umma wa Watanzania kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Taifa. Tano, Wizara inaimarisha moyo wa uzalendo na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa vijana wa Kitanzania na kuwaandaa kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali ili kukuza moyo wa kujitegemea. Sita, Wizara inafanya utafiti na kuendeleza teknolojia kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kiraia. Saba, Wizara inasaidia kuimarisha amani na utengamano na nchi nyingine duniani hasa nchi jirani.

MALENGO YA WIZARA

9. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilikusudia kutekeleza malengo manane katika mwaka 2011/2012. Kwanza, Wizara iliandikisha wanajeshi wapya na kuimarisha mafunzo na mazoezi ya kijeshi. Pili, Wizara iliimarisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana wa kujitolea. Tatu, Wizara iligharamia huduma muhimu ikiwemo umeme, maji, simu, mafuta na vilainisho kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu ya msingi. Nne, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliwapatia chakula, tiba na sare za wanajeshi, vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na Watumishi raia. Tano, Wizara iliendeleza ushirikiano na nchi nyingine duniani katika nyanja za kijeshi. Sita, Wizara ilinunua zana na vifaa mbalimbali vya kijeshi. Saba Wizara ilitekeleza mradi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia silaha na milipuko. Nane Wizara pia ilijenga na kukarabati baadhi ya majengo na miundombinu katika makambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa.

HALI YA USALAMA WA MIPAKA KATIKA MWAKA 2011/2012

10. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jukumu kuu la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru na maslahi ya taifa (vital national interests), naomba sasa nielezee hali ya ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi yetu katika mwaka 2011/2012. Katika kipindi hiki hali ya ulinzi na usalama wa mipaka yetu na nchi jirani ilikuwa shwari. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kudhibiti ipasavyo ulinzi wa mipaka yote ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa salama. Aidha, matukio ya uharamia katika eneo letu la Mwambao wa Bahari ya Hindi yalipungua. Kwa jumla kulikuwa na tukio moja tu la utekaji wa meli na majaribio matatu ya kutaka kuteka meli ukilinganisha na mwaka 2010/2011 ambapo meli nne zilitekwa na kulikuwa na majaribio 10 ya kutaka kuteka meli. Jeshi liliwakamata maharamia hao na kuwakabidhi kwa vyombo vya dola kwa hatua za kisheria. Katika kipindi hiki vurugu katika baadhi ya nchi jirani zimesababisha ongezeko la wahalifu wanaoingia nchini wakiwa na silaha kwa lengo la kufanya vitendo vya ujambazi. Jeshi la Wananchi linaendelea kuimarisha ulinzi wa maeneo ya mipaka inayozunguka nchi yetu ili kudhibiti vitendo hivyo.

(I) MPAKA KATIKA BAHARI YA HINDI

11. Mheshimiwa Spika, mpaka katika bahari ya Hindi una urefu wa kilomita 1,424. Katika mpaka huu Tanzania inapakana na nchi za Kenya, Visiwa vya Ushelisheli, Komoro na Msumbiji. Hali ya usalama katika mpaka wa Bahari ya Hindi ilikuwa nzuri. Matukio ya vitendo vya uharamia yameanza kupungua kufuatia operesheni zinazofanywa na Jeshi letu la Wanamaji katika eneo la Bahari ya Hindi. Serikali pia inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti vitendo vya uharamia katika mipaka yetu kwa kuimarisha uwezo wa Jeshi letu kiutendaji ili liweze kupambana na maharamia hao kikamilifu.

(II) MPAKA WA KASKAZINI

12. Mheshimiwa Spika, katika mpaka wa Kaskazini Tanzania imepakana na Kenya na Uganda. Hali ya usalama wa mpaka wetu wa kaskazini kwa ujumla imekuwa shwari. Hata hivyo, kumejitokeza tatizo la ung’oaji wa alama za mipakani (beacons) unaofanywa na watu wanaoishi kwenye mpaka kwa lengo la kujipatia ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho ya mifugo na ujenzi wa makazi. Hapana shaka tatizo hili linatishia usalama wetu. Serikali inafanya mipango ya kurudisha alama hizo za mipakani. Vile vile Serikali inafanya uchambuzi wa gharama zinazohitajika katika ujenzi wa barabara za usalama mipakani (Security roads). Lakini kutokana na ukubwa wa kazi hii Serikali haitaweza kuitekeleza mara moja. Kazi ya ujenzi wa barabara za usalama mipakani itatekelezwa kwa awamu kwa kuanzia na maeneo ya mpakani yenye matishio mengi ya usalama ikiwemo mpaka wa Magharibi. Wakati Serikali yetu ikiendelea kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hili ninawasihi wananchi hasa wale wanaoshi katika maeneo ya mipakani kuheshimu na kuzitunza alama za mipaka kwa sababu alama hizi zina umuhimu mkubwa katika kudumisha ulinzi.

(III) MPAKA WA MAGHARIBI

13. Mheshimiwa Spika, katika mpaka wa Magharibi Tanzania inapakana na Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hali ya usalama katika eneo la mpaka huu ni ya wastani. Hata hivyo, kumekuwepo na matukio ya ujambazi yanayofanywa na watu wenye silaha wanaodhaniwa wanatoka katika nchi jirani hasa Kongo na Burundi. Majambazi haya yamekuwa yakiwashambulia wavuvi na kuwanyang’anya vifaa vya uvuvi na wakati mwingine kuwaua. Mnamo mwezi Mei, 2012 majambazi yenye silaha za kivita kutoka nchi jirani waliwapora wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika, kufanya mauaji na kuwajeruhi askari. Tukio hili ni muendelezo wa matukio ya ujambazi yanayofanywa kwenye Ziwa Tanganyika. Jeshi la Wananchi wa Tanzania linaendelea kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na vitendo hivyo vya ujambazi katika Ziwa Tanganyika. Katika kukabiliana na matukio hayo Serikali inafanya mipango ya kuipatia Kamandi ya Jeshi la Wanamaji meli na boti ziendazo kasi za kufanyia doria baharini na maziwa makubwa hasa ziwa Tanganyika. Kwa nchi kavu jeshi katika eneo la ziwa Tanganyika tayari limeanza utaratibu wa kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.

(IV) MPAKA WA KUSINI

14. Mheshimiwa Spika, katika mpaka wa Kusini Tanzania inapakana na Msumbiji, Malawi na Zambia. Hali ya usalama katika mpaka huu imeendelea kuwa shwari. Hata hivyo, hivi karibuni zimejitokeza dalili za kuhatarisha usalama wa mpaka huo hasa kwenye eneo la Ziwa Nyasa. Serikali imeiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutumia njia za kidiplomasia ili kulipatia suala hili ufumbuzi wa kudumu.

15. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa viashiria vya kuhatarisha usalama katika baadhi ya maeneo ya mipakani napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi wote kwa jumla kwamba Jeshi letu limejiandaa vyema na lina uwezo mkubwa wa kukabiliana na tishio la aina yoyote dhidi ya Uhuru na Usalama wa nchi yetu.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2011/2012

16. Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitoe taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilikusudia kutekeleza malengo ya mpango mkakati wa kuimarisha utendaji na maslahi ya Wanajeshi kwa kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi 2024/2025. Utekelezaji wa bajeti pia ulizingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 inayosisitiza umuhimu wa kujenga Jeshi dogo la kisasa, shupavu na lenye weledi wa hali ya juu.

17. Mheshimiwa Spika, ili kufikia azma hiyo bajeti ya mwaka 2011/2012 ililenga katika kununua zana na vifaa mbalimbali vya kijeshi, kujenga maghala ya kisasa ya kuhifadhia silaha na milipuko, kukarabati na kujenga nyumba za makazi katika makambi, shule, vyuo na ofisi. Aidha, bajeti hiyo ilidhamiria kuimarisha malipo ya mishahara, posho, mavazi, usafiri na huduma za matibabu. Kwa ujumla utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2011/2012 ulikuwa kama ifuatavyo:-

18. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwisho wa mwezi Aprili, 2012 Mafungu ya Wizara hii yalikusanya mapato ya shilingi 47,123,636.00 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi 28,355,000.00. Sehemu kubwa ya makusanyo haya ni maduhuli kutokana na mauzo ya nyaraka za zabuni na mapato kutokana na shughuli za mafunzo kwa vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (Kiambatisho Na. 1).

19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliidhinishiwa bajeti ya shilingi 682,315,415,000 ambazo kati yake shilingi 533,396,593,000 sawa na asilimia 80 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 148,918,822,000.00 sawa na asilimia 20 kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

20. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2012 Wizara yangu ilipatiwa shilingi 797,251,016,700.00 sawa na asilimia 117 ya bajeti iliyoidhinishwa yaani shilingi 682,315,415,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 653,551,016,700.00 zilitumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 122 ya fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya shughuli hizo. Kuongezeka kwa matumizi hayo kulitokana na fungu 38 NGOME na fungu 39 JKT kuongezewa fedha kwa ajili ya kugharamia madeni ya uhamisho, likizo na posho za wanajeshi. Vile vile fungu 57 Wizara ya Ulinzi liliongezewa fedha kwa ajili ya malipo ya mishahara kwa mwezi Mei na Juni, 2012 kwa sababu bajeti ya mishahara katika fungu hili ilifikia ukomo katika mwezi Aprili, 2012. Fedha zilizotolewa na kutumika kwa ajili ya shughuli za Matumizi ya Maendeleo zilikuwa shilingi 143,700,000,000.00 sawa na asilimia 96 ya shilingi 148,918,822,000.00 zilizoidhinishwa kwa ajili ya shughuli hizo. Kwa hiyo kiasi cha shilingi 5,218,822,000.00 kilichoidhinishwa kwa shughuli za maendeleo hakikutolewa. Mchanganuo wa bajeti na matumizi hayo umeonyeshwa kwenye mafungu matatu ya Wizara. (Kiambatisho Na. 2)

(I) MAFUNZO NA MAZOEZI YA KIJESHI KWA WANAJESHI

21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Jeshi la Ulinzi limewapatia mafunzo maafisa na askari ili kuwawezesha kumudu vyema kuzitumia silaha, zana na vifaa vya kijeshi zinazotumika katika kutekeleza majukumu ya Ulinzi wa Taifa. Vile vile maafisa na askari walipatiwa kozi katika vyuo na vituo vya mafunzo ndani na nje ya nchi. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lina jumla ya maafisa na askari 672 katika Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu nchini na 113 wanaosoma kozi za kijeshi nje ya nchi. Jeshi la Ulinzi pia lilishiriki katika mazoezi ya pamoja na majeshi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi katika Jumuiya hiyo. Halikadhalika, Jeshi lilifanya mafunzo mawili. Kwanza, Jeshi liliandaa zoezi la NATURAL FIRE -11 lililofanyika mwezi Septemba, 2011 huko Zanzibar. Pili, Jeshi lilifanya zoezi la USHIRIKIANO IMARA lililofanyika mwezi Oktoba, 2011 nchini Rwanda.

(II) MAFUNZO KWA JESHI LA AKIBA

22. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi limeendelea kuendesha mafunzo ya awali na uongozi mdogo kwa mgambo hapa nchini. Mafunzo ya mgambo yaliendeshwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara ambapo wananchi 12,825 walipata mafunzo hayo. Vilevile wanamgambo 40 walipewa mafunzo ya uongozi mdogo ili kupata ujuzi wa kuwasimamia na kuwaongoza wanamgambo walio chini yao.

(III) UNUNUZI WA ZANA NA VIFAA VYA KIJESHI

23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kuelekeza mkakati wa kuimarisha Jeshi la Wananchi kwa kulinunulia zana na vifaa vya kisasa. Miongoni mwa zana hizo zilizonunuliwa ni zile tulizozionesha kwenye uwanja wa Uhuru siku ya kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 09 Desemba, 2011. Aidha, kupitia mkakati huo, Kamandi ya Jeshi la Anga limepatiwa zana na vifaa muhimu ili kuimarisha utendaji kazi. Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu pia ilipatiwa zana na vifaa vipya.

(IV) MATENGENEZO NA UKARABATI WA ZANA NA VIFAA

24. Mheshimiwa Spika, kama mnavyoelewa gharama za ununuzi wa zana za kijeshi na ukarabati wake ni kubwa sana ukilinganisha na uwezo wa kifedha tuliokuwa nao. Serikali imeweza kugharamia asilimia 20 ya mahitaji ya ukarabati na ununuzi wa zana mpya katika mwaka 2011/2012. Kwa kutambua umuhimu wa suala hili, Serikali inafanya juhudi ya kutafuta fedha kutekeleza mpango maalum wa matengenezo na ukarabati wa zana na vifaa vya jeshi letu kwa kutumia taasisi yetu ya Nyumbu. Mpango huu ni muhimu hasa ukizingatia kwamba uwezo wetu wa kununua vifaa na zana mpya ni mdogo kama nilivyosema hapo awali.

(V) USHIRIKIANO WA KIULINZI NA KIJESHI NA NCHI NYINGINE DUNIANI

25. Mheshimiwa Spika, ushirikiano kati ya nchi yetu na nchi nyingine katika nyanja za kijeshi ni suala muhimu katika kudumisha usalama na amani Duniani. Katika mwaka 2011/2012, ushirikiano huo ulitekelezwa kupitia ushirikiano baina ya nchi na nchi (bilateral cooperation), ushirikiano wa kikanda (regional cooperation) na ushirikiano wa kimataifa (multilateral cooperation).

26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kudumisha ushirikiano katika nyanja za kijeshi baina ya nchi yetu na nchi nyingine. Nchi tunazoshirikiana nazo ni pamoja na Canada, China, India, Jordan, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu. Katika kuimarisha ushirikiano huo, Wizara inakusudia kufungua ofisi mpya za Waambata wa Jeshi katika nchi za Malawi, Ujerumani na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ushirikiano baina ya nchi yetu na nchi nilizozitaja umejikita katika upatikanaji wa zana na vifaa, mafunzo na mazoezi ya kijeshi, misaada ya tiba, mafunzo ya ulinzi wa amani, mapambano dhidi ya uharamia, utafiti, uchunguzi wa milipuko katika makambi, teknolojia na michezo. Napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali na Majeshi ya nchi hizo kwa ushirikiano mzuri waliotupatia.

27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kijeshi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kudumisha amani katika ukanda huu. Ushirikiano na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea katika nyanja za mafunzo, mazoezi ya pamoja na michezo baina ya majeshi ya nchi hizo. Majeshi yetu pia yamekuwa yakibadilishana taarifa za kiulinzi na usalama. Vile vile kupitia ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi na Nchi za SADC tarehe 07 Februari, 2012 nchi yetu ilisaini makubaliano ya ulinzi wa pamoja kwenye Bahari ya Hindi na nchi za Afrika Kusini na Msumbiji ikiwa ni jitihada za kukabiliana na tatizo la uharamia.

28. Mheshimiwa Spika, nchi yetu inao wajibu mkubwa katika kushirikiana na nchi nyingine ili kudumisha amani duniani. Nchi yetu imekuwa ikishiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa katika nchi zenye migogoro. Mpaka sasa Jeshi letu la Ulinzi limepeleka jumla ya wanajeshi 1,081 kushiriki operesheni za Ulinzi wa Amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ivory Coast, Lebanon na Darfur – Sudan. Kutokana na utendaji mzuri wa vikundi vyetu vya Ulinzi wa Amani, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeiomba Serikali ya Tanzania kupeleka waangalizi wa amani kati ya 100 na 200 nchini Syria. Serikali imekubali ombi hilo. Hivi sasa Makao Makuu ya Jeshi yanafanya maandalizi ya kuwapeleka waangalizi hao Syria ili waweze kushiriki kwenye operesheni hiyo. Kutokana na uwezo mkubwa wa Makamanda wa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa miongoni mwa Makamanda wa ngazi za juu wa Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyopo huko Darfur-Sudan mmoja ni Mtanzania aliyekuwa Kamanda wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ya Jeshi letu la Ulinzi, Meja Jenerali Wynjones Kisamba. Meja Jenerali Kisamba ni Naibu Kamanda wa vikosi hivyo.

29. Mheshimiwa Spika, pamoja na shughuli za Ulinzi wa Taifa Jeshi la Wananchi pia linatekeleza shughuli za viwanda. Shirika la Mzinga limekamilisha mradi wa ukarabati na uboreshaji wa kiwanda awamu ya kwanza. Shirika hili limeweka mitambo na kuwapatia mafunzo waendeshaji wa mitambo hiyo. Mradi huo ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 16 Januari, 2012. Shirika linaendelea kufanya utafiti wa zana za kijeshi pamoja na kuzifanyia ukarabati ili zitumike katika hali ya usalama. Halikadhalika, Shirika la Mzinga limebuni vyanzo vya ziada vya kuliongezea mapato. Vyanzo hivyo ni pamoja na kuanzisha kampuni tanzu ya Mzinga Holdings itakayoshughulikia ujenzi na uendeshaji wa maduka yasiyotozwa ushuru (duty free shops) katika vikosi vya Jeshi.

30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 Shirika la Nyumbu kwa upande wake limeendelea kutekeleza mpango wa muda mrefu (2010 - 2025) wenye malengo ya kufanya utafiti na uvumbuzi katika teknolojia za magari na mitambo, kuzalisha na kusambaza magari na mitambo ili kulifanya Shirika hili kuwa kituo kilichotukuka katika masuala ya teknolojia (centre of excellence) Afrika Mashariki. Shughuli zilizofanyika katika kutekeleza mpango huo ni pamoja na kuendeleza teknolojia za kilimo, kuimarisha uwezo wa kituo katika uzalishaji wa vipuri na kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa kujenga kituo maalum cha kuhakiki ubora wa vifaa vinavyotengenezwa. Hata hivyo, Shirika halikuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa sababu halikutengewa fedha za maendeleo.

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012 Jeshi limetekeleza miradi kadhaa ya ujenzi wa majengo ya vyuo na shule za kijeshi hususan Chuo cha Unadhimu na Ukamanda (Tengeru, Arusha), Shule ya Kijeshi ya Ulinzi wa Anga (Tanga), shule ya Usalama na Utambuzi wa Kijeshi (Mbagala, Dar es Salaam), Chuo cha Ulinzi wa Taifa (Kunduchi, Dar es Salaam) na ujenzi wa Maktaba katika Chuo cha Kijeshi Monduli (Arusha). Aidha, miradi ya ujenzi wa maghala bora ya kisasa ya kuhifadhia silaha na milipuko nayo imeanza.

32. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuimarisha mafunzo ya maafisa wa juu wa Jeshi na maafisa waandamizi wa Serikali ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, ujenzi wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa umekamilika na kinategemea kuanza kutoa mafunzo mwezi Septemba, 2012. Kozi ya kwanza itakuwa mahsusi kwa wanafunzi kutoka Tanzania pekee. Baada ya kupata uzoefu kutokana na uendeshaji wa kozi ya kwanza, Chuo kitaalika wanafunzi wenye sifa zinazolingana na hizo kutoka nchi jirani. Kozi zote zitaendeshwa kwa ushirikiano kati yetu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kuboresha Mtandao wa Mawasiliano Jeshini. Wizara inaendelea kuboresha mtandao huu kwa kuondoa mitambo ya zamani iliyochakaa na kuweka mitambo mipya na ya kisasa vikosini. Mradi huu umetekelezwa katika vikosi vilivyoko katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

34. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi ikiwa ni pamoja na stahili na huduma muhimu. Katika mwaka, 2011/2012 mishahara ya askari ilipandishwa na posho ya chakula pia iliyopandishwa kutoka shilingi 5,000 hadi 7,500 kwa siku. Madeni ya wanajeshi yenye jumla ya shilingi 43,201,205,416.00 pia yalilipwa. Halikadhalika, madeni ya wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali jeshini yenye thamani ya shilingi 24,248,160,000.00 (wakiwemo TANESCO na mamlaka za Maji) yalilipwa. Aidha, katika mwaka 2011/2012 huduma ya mavazi iliboreshwa kwa wanajeshi kupatiwa sare mpya.

35. Mheshimiwa Spika, huduma ya tiba kwa wanajeshi na familia zao, vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na Watumishi raia ndani ya Jeshi, imeendelea kutolewa kwa kutumia vituo visivyopungua 70 nchi nzima. Hospitali za Jeshi za Kanda na hospitali za Lugalo, Nyumbu (Kibaha), Mwanza na Tabora zimeimarishwa. Hospitali hizi zina wahudumia wanajeshi na raia wanaoishi karibu na maeneo ya kambi.

36. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendeleza ujenzi wa nyumba za makazi ya maafisa na askari vikosini, pamoja na ujenzi mpya wa majengo mbalimbali. Sambamba na uendelezaji wa ujenzi wa majengo hayo, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeridhia kutoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Kimarekani 285,000,000 kwa ajili ya mpango wa ujenzi wa nyumba za kuishi maafisa na askari vikosini. Serikali imekamilisha taratibu za upatikanaji wa mkopo huo kupitia Benki ya Exim ya China. Mkataba wa mkopo umetiwa saini tarehe 20 Juni, 2012 na ujenzi unatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni.

37. Mheshimiwa Spika, Jeshi la wananchi lilishiriki katika kukabiliana na majanga, zikiwemo operesheni ya kuokoa watu na mali, kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokea mkoani Dar es Salaam mwezi, Desemba, 2011 na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander huko Nungwi Unguja mwezi Septemba, 2011. Jeshi pia limetekeleza na kukamilisha zoezi la usombaji wa mahindi tani 5,000 kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, tani 10,000 kutoka Songea kwenda Makambako, na tani 5,000 kutoka Makambako na Iringa kwenda Dar es Salaam. Jeshi pia limepewa kazi ya kusomba tani 30,000 za mahindi kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda na Mbozi. Utekelezaji wa zoezi hili unasubiri upatikanaji wa fedha.

(VI) MAFUNZO YA VIJANA WA JKT

38. Mheshimiwa Spika, umoja wa kitaifa miongoni mwa wananchi ni jambo muhimu katika kuimarisha ulinzi wa Taifa letu. Kwa kutambua umuhimu wa suala hili, Serikali inaendelea kuwajengea vijana wa Kitanzania moyo wa utaifa, ukakamavu na ujasiri kwa kuwapatia mafunzo ya uzalendo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa. Katika mwaka 2011/2012 vijana wa kujitolea 5,844 wamehitimu mafunzo ya awali ya JKT. Kati yao wavulana walikuwa 4,554 na wasichana 1,290. Mafunzo hayo yaliendeshwa katika makambi nane ya Msange, Kanembwa, Ruvu, Oljoro, Mgambo, Mafinga, Mlale na Bulombora. Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, vijana hao wameendelea na mafunzo ya stadi za kazi katika vyuo vya ufundi vilivyopo katika makambi ya Mgulani, Makutupora, Nachingwea, Mlale, Msange, Bulombora, Mafinga, Maramba, Kanembwa, Mgambo, Rwamkoma, Oljoro na Chita. Kati ya vijana 5,844 waliopatiwa mafunzo vijana 3,406 walifanikiwa kupata ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na mashirika mbalimbali. Wizara ya Ulinzi imeamua kutumia utaratibu wa kuajiri vijana wanaotaka kujiunga na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka kwenye JKT na JKU ili kupata vijana wazalendo na wenye nidhamu.

39. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga Taifa limefanya ukarabati wa majengo mbali mbali ili yaweze kutumiwa na vijana wa kujitolea. Ukarabati huo umefanyika katika makambi ya Bulombora na Kanembwa (Kigoma), Mafinga (Iringa), Makutopora (Dodoma), Mgambo (Tanga), Mlale (Ruvuma), Msange (Tabora), Oljoro (Arusha), Ruvu (Pwani) na Rwamkoma (Mara). Hivi sasa makambi haya yana uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja. Vilevile Jeshi la Kujenga Taifa limeyakarabati makambi ya Chita (Morogoro), Maramba (Tanga), Mbweni na Mgulani (Dar es Salaam), Itende (Mbeya) na Nachingwea (Lindi) ili yaweze kutoa mafunzo ya stadi za kazi na maisha.

40. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Kujenga Taifa limekarabati mahanga mapya ya vijana vikosini kwa ajili ya mafunzo ya awali na ukarabati wa nyumba za maafisa, askari na watumishi raia wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Aidha, ukarabati wa zahanati moja na ujenzi wa jengo la Utawala la Chuo cha Uongozi Kimbiji ulikamilika. Vile vile, miundombinu katika vikosi vya Kanembwa na Nachingwea iliimarishwa sambamba na upimaji wa eneo la vikosi hivyo.

(VII) SHUGHULI ZA SHIRIKA LA SUMAJKT

41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, Shirika la SUMAJKT lilipata kazi mbalimbali zenye thamani ya shilingi 10,615,667,122.00 na kupata faida ya shilingi 1,232,726,924.00. Mapato yaliyopatikana katika kazi hizi yametumika kununulia vifaa kama vile magari na vifaa vya ofisini. Aidha, kutokana na utendaji wake mzuri shirika hili limeendelea kupata kazi mbalimbali. Shirika hili limetoa ajira kwa vijana zaidi ya mia tisa kwa ajili ya shughuli za viwanda, kilimo, ujenzi na ulinzi kupitia kampuni tanzu ya SUMA Guard.

42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/2012, SUMAJKT ilitekeleza mradi wa uunganishaji na uuzaji wa matrekta 1,846 na zana zake 1,450. Matrekta na zana hizi zilinunuliwa kwa mkopo kutoka Serikali ya India. Hadi kufikia tarehe 09 Julai, 2012 SUMAJKT ilikuwa imeuza matrekta 786. Katika kusogeza matrekta karibu na wateja wake, SUMAJKT imefungua vituo vya kuuzia matrekta hayo katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza na Arusha. Nimemwagiza wakala wa uuzaji wa matrekta kufanya mipango ya kuyahamishia matrekta yaliopo Mwenge Dar es Salaam na kuyapeleka Morogoro. Shirika la SUMAJKT linatarajia kufungua vituo zaidi vya mauzo ya matrekta kupitia kwa Wakuu wa Mikoa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kama vile ushauri na vipuri. Juhudi za kuyatangaza matrekta hayo zinaendeshwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo vipindi maalum kwenye Televisheni.

43. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa matrekta katika kuendeleza Kilimo Kwanza, Serikali imepunguza bei ya matrekta ambapo matrekta yenye “horse power” 50 yaliyokuwa yakiuzwa shilingi milioni 25.6 sasa yanauzwa shilingi milioni 16.5 na matrekta yenye “horse power” 70 yaliyokuwa yanauzwa shilingi milioni 45.8 sasa yanauzwa shilingi milioni 38.8. Hivi sasa Shirika linawapunguzia wateja malipo ya awali (down payment) kutoka asilimia 50 ya bei ya trekta moja hadi asilimia 30. Vile vile Shirika linafikiria kupunguza zaidi malipo ya awali hadi asilimia 15 kwa wateja watakaonunua matrekta kuanzia 50 na kuendelea. Halikadhilika, Halmashauri za Wilaya ambazo zitakuwa tayari kuwadhamini wakulima wadogo wadogo imependekezwa zilipe malipo ya awali ya asilimia 10.

44. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, Jeshi la Kujenga Taifa limeendelea kutekeleza jukumu la uzalishaji wa mazao ya chakula, biashara na mazao ya mbegu bora za nafaka. Katika mwaka 2011/2012, JKT limezalisha tani 356 za mazao ya chakula na biashara na linakadiria kuvuna tani 1,511 za mbegu bora za mazao mbalimbali. Mbegu hizo zitauzwa kwa Wakala wa Mbegu “Agriculture Seed Agency” na kampuni binafsi ya “Sourthen Highland Seeds Growers”, Kampuni zenye mkataba na JKT katika uzalishaji mbegu. Aidha, ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa awamu ya kwanza unaendelea katika kikosi cha Chita. Ujenzi huo utakapokamilika utasaidia kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa ekari 1,000 za zao la mpunga. Upanuzi wa kilimo hicho utaendelea hatua kwa hatua kadri fedha zitakavyopatikana. JKT ina lengo la kuendeleza ekari 30,000 za kilimo cha umwagiliaji katika kikosi hicho cha Chita.

45. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ufugaji wa kisasa, JKT limeanza kutekeleza uzalishaji wa ng’ombe wa kisasa kwa njia ya chupa (artificial insermination) ambapo wataalamu wa fani hiyo wamepatiwa mafunzo katika Chuo cha Uhamilishaji Arusha (National Artificial Insermination Centre) huko Usa River, Arusha. JKT pia ina mpango wa kuanzisha kliniki ya mifugo na kituo cha ukusanyaji mbegu za madume bora ya Ng’ombe wa maziwa na nyama.

(VIII) HIFADHI YA MAZINGIRA

46. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya kuimarisha Mazingira. Katika mwaka 2011/2012 elimu ya utunzaji mazingira imeendelea kutolewa kwa vijana wa JKT, watumishi raia na wananchi wanaoishi jirani na makambi. Kazi ya upandaji miti katika makambi inaendelea. Aidha, baadhi ya vikosi vilishiriki katika kuwania tuzo ya Rais ya kuhifadhi vyanzo vya maji, kupanda na kutunza miti. Vikosi vya Kaboya (Kagera), Ruvu (Pwani) na Maramba (Tanga) vilipata ushindi ki-mkoa. Pia vikosi vyetu vimeshiriki katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira Duniani kwa kushiriki kwenye kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya usafi, kupanda miti na kutoa elimu ya mazingira.

CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2011/2012

47. Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita, changamoto kubwa iliyoikabili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika kutekeleza mpango na bajeti ya mwaka 2011/2012 ni kupatiwa kiwango kidogo cha ukomo wa bajeti ukilinganisha na mahitaji halisi ya Mafungu ya Wizara hii. Hali hii imeathiri sana utekelezaji wa mipango muhimu ya miradi ya maendeleo kama vile ununuzi wa zana na vifaa, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia silaha na milipuko, ujenzi na ukarabati wa majengo ikiwemo nyumba za makazi katika makambi, uboreshaji wa viwanda vya utafiti na uzalishaji wa bidhaa za kijeshi.

48. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Matumizi ya Kawaida hali hiyo imeathiri shughuli nyingi muhimu ikiwemo ulipiaji wa huduma na mahitaji muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu kama vile mafuta, maji, umeme na stahili za Wanajeshi na Watumishi raia. Shughuli nyingine zilizoathirika ni utoaji wa huduma ya tiba, ushiriki katika jumuiya za kikanda katika nyanja za kijeshi na uendeshaji wa ofisi zetu za Waambata Jeshi katika nchi za nje. Kwa jumla, hali hiyo inasababisha malimbikizo ya madeni licha ya Serikali kuchukua hatua za kupunguza madeni haya.

49. Mheshimiwa Spika, vile vile Wizara inakabiliwa na tatizo la kuchelewa kupokea fedha kutoka HAZINA kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Hali hii imesababisha mipango kazi ya utekelezaji wa miradi kuvurugika na wakati mwingine kukiuka mikataba ya kimataifa na hivyo kuzua manung’uniko kutoka kwa wadai na kutishia kutushitaki mahakamani kwa kuvunja makubaliano ya mikataba hiyo.

MIGOGORO YA ARDHI BAINA YA JESHI NA WANANCHI

50. Mheshimiwa Spika, halikadhalika, Wizara yangu inakabiliwa na migogoro ya ardhi. Wakati wa kuhitimisha hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2011/2012, pamoja na mambo mengine, nililiarifu Bunge lako Tukufu kuwa nimeunda Kikosikazi cha kushughulikia migogoro hiyo katika maeneo yote nchini. Kufuatia hatua hiyo, tumeweza kubainisha matatizo yafuatayo:-

(i) Migogoro mingi ya ardhi kati ya jeshi na wananchi inatokana na maeneo kutopimwa na kupewa hati za umiliki.

(ii) Baadhi ya wananchi wanavamia maeneo ya Jeshi hasa maeneo yenye vishawishi vya kimaendeleo kama vile kilimo, makazi na uwekezaji.

(iii) Baadhi ya wananchi hawaheshimu alama za mipaka ya maeneo na hata kung’oa kwa makusudi alama hizo kwa nia ya kuvamia maeneo hayo.

(iv) Baadhi ya wananchi hawaelewi umuhimu wa jeshi kumiliki maeneo makubwa kwa matumizi ya kijeshi.

51. Mheshimiwa Spika, ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hili Wizara imeanza kuchukua hatua mbalimbali. Katika baadhi ya maeneo tutalazimika kuwaondoa wavamizi mara moja ili kupisha shughuli za jeshi. Aidha, kwa maeneo ambayo uingiaji wa watu umezidi kiwango kiasi cha kufanya eneo husika kutokufaa tena kwa shughuli za Jeshi, tutashauriana na mamlaka zinazohusika kuangalia uwezekano wa kupewa maeneo mbadala kama tulivyofanya katika eneo la Kikosi cha 977 Tanganyika Packers huko Arusha. Eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2495 lilitengwa kwa mafunzo ya mizinga na makombora. Hata hivyo, baada ya uvamizi mkubwa uliofanywa na wananchi, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameridhia tupime na kurekebisha mipaka upya. Kwa msingi huo jeshi limepewa eneo mbadala la Themi Holdings Grounds huko Arusha. Ninatoa wito kwa waheshimiwa wabunge na wananchi kwa ujumla kuheshimu maeneo yanayomilikiwa na JWTZ. Jeshi lipo kwa sababu wananchi wa Tanzania wapo. Katika Dunia ya leo ambayo inatawaliwa sana na tamaa ya kujipatia maslahi ya kiuchumi hatuwezi kuishi bila Jeshi. Wizara itaendelea kuchukua hatua ya kulinda maeneo hayo. Nawaomba Viongozi wote tushirikiane katika kutatua matatizo hayo ili kuepuka migororo isiyokuwa ya lazima.

MAFUNZO YA JESHI LA KUJENGA TAIFA KWA MUJIBU WA SHERIA

52. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2011/2012, Wizara yangu iliahidi kwamba itarejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mujibu wa Sheria. Maandalizi ya kuanza zoezi hilo yamekamilika ambapo JKT wako tayari kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, gharama za kuendeshea mafunzo hayo ni kubwa. Kwa hiyo hatutaweza kuchukua vijana wote wanaostahili kupitia JKT kwa Mujibu wa Sheria. Kutokana na hali hiyo Serikali inapanga kurejesha mafunzo hayo kwa majaribio ya vijana 5,000. Vijana hao ni miongoni mwa vijana 41,348 ambao watahitimu mafunzo ya Kidato cha Sita katika mwaka 2013.

53. Mheshimiwa Spika, kupata vijana 5,000 kati ya vijana 41,348 ni kazi kubwa. Kwa hivyo, Wizara imeweka vigezo maalum vya kuwapata vijana hao kwa kuzingatia makundi. Makundi ya vijana hao yatatangazwa mwezi Januari 2013.

54. Mheshimiwa Spika, mafunzo hayo yanategemea kuanza mwezi Machi, 2013 na yatafanyika kwa miezi sita katika makambi ya Bulombora na Kanembwa (Kigoma), Mlale (Ruvuma), Mafinga (Iringa), Msange (Tabora) na Oljoro (Arusha). Mpango wa utekelezaji wa jukumu hili utakuwa kama ifuatavyo:-

(i) Kuandikisha vijana kutoka shuleni kuanzia mwezi Desemba, 2012 hadi Januari, 2013. (ii) Kuwapokea vijana katika makambi kuanzia tarehe 07 hadi 16 Machi, 2013. (iii) Kuanza Mafunzo ya awali tarehe 17 Machi, 2013.

(iv) Mwisho wa Mafunzo tarehe 16 Agosti, 2013

55. Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara yangu ya mwaka 2011/2012 pamoja na mambo mengine tulipokea ombi la wabunge vijana kuandaliwa mafunzo maalum ya Jeshi la Kujenga Taifa. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imelifanyia kazi ombi hilo na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalum ya wiki tatu kwa waheshimiwa Wabunge vijana. Mafunzo haya yataanza mwezi Machi, 2013 sanjari na kuanza rasmi kwa mafunzo ya vijana kwa Mujibu wa Sheria. Kwa hivyo Waheshimiwa Wabunge vijana wataungana na kundi la kwanza la vijana 5,000 niliowaeleza hapo juu. Ni imani yetu kuwa pamoja na Waheshimiwa Wabunge kunufaika na mafunzo hayo, watahamasisha zoezi la urejeshwaji wa mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria na kutoa taswira nzuri ya mafunzo haya kwa jamii. Naomba Waheshimiwa Wabunge mjiorodheshe kwa maandalizi ya mafunzo haya.

MALENGO YA MWAKA 2012/2013

56. Mheshimiwa Spika, mpango wa mwaka 2012/2013 umelenga kuendeleza juhudi zilizofanyika za kuliimarisha Jeshi pamoja na kutoa huduma mbalimbali kwa wanajeshi na Watumishi raia. Malengo ya mpango huo yatazingatia utekelezaji wa shughuli zifuatazo:-

a.MATUMIZI YA KAWAIDA

(i) Kuandikisha wanajeshi wapya na kuimarisha mafunzo na mazoezi ya kijeshi ikiwa ni pamoja na kushiriki katika mazoezi ya pamoja na majeshi ya nchi nyingine na mafunzo ya Ulinzi wa mgambo.

(ii) Kuimarisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana wa Kitanzania wa kujitolea.

(iii) Kugharamia upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo umeme, maji, simu, mafuta na vilainisho.

(iv) Kutengeneza na kukarabati magari, vifaa, mitambo na zana za kijeshi.

(v) Kutoa huduma muhimu kwa Wanajeshi na Vijana wa JKT ikiwemo chakula, tiba, sare na usafiri.<.p>

(vi) Kulipa stahili mbalimbali za Wanajeshi, Vijana wa JKT na Watumishi raia.

(vii) Kuendeleza shughuli za ushirikiano na nchi nyingine duniani katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.

(viii) Kurejesha Utaratibu wa Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mujibu wa Sheria.

b. MATUMIZI YA MAENDELEO

(i) Kuimarisha Jeshi la Ulinzi kwa kulipatia zana na vifaa bora. (ii) Kuendelea na ujenzi maghala ya kuhifadhia zana na vifaa vya Jeshi.

(iii) Kukarabati mitambo na miundombinu katika viwanda na vituo vya utafiti na uendelezaji wa

teknolojia ya kijeshi.

(iv) Kukarabati na kuendeleza ujenzi wa majengo na miundombinu katika makambi ya jeshi.

SHUKURANI

57. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru watu mbalimbali kwa michango waliyoitoa katika kutayarisha makadirio haya. Nawashukuru Katibu Mkuu Bw. Job D. Masima, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Mussa I. Iyombe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Samuel A Ndomba, Meneja Mkuu Shirika la Mzinga Brigedia Jenerali Dkt. Charles Muzanila na Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumbu Kanali Anselm Bahati.

58. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo (Makao Makuu ya Wizara), Wakuu wa Matawi (NGOME), Wakuu wa Idara (Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa), Makamanda wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Anga na Jeshi la Wanamaji, Maafisa, Askari na Watumishi wote raia wanaofanya kazi chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Vile vile namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Mwisho nawashukuru wafanyakazi wote wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika kuongoza Wizara hii tangu tarehe 10 Mei, 2012 nilipofika rasmi Wizarani hapo.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/2013

59. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2012/2013 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekadiria kukusanya mapato kiasi cha shilingi 57,650,000.00 katika mchanganuao ufuatao:-

a. Fungu 38 NGOME -shilingi 2,650,000.0

b. Fungu 39 – JKT shilingi 30,000,000.00

c. Fungu 57- ULINZI shilingi 25,000,000.00

Jumla shilingi 57,650,000.00

60. Mheshimiwa Spika, ili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iweze kutekeleza malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2012/2013, naomba Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha jumla ya shilingi 1,086,550,058,000.00 ambazo kati yake shilingi 678,363,492,000.00 zitatumika kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na shilingi 408,186,566,000.00 ni bajeti ya matumizi ya maendeleo.

 61. Mheshimiwa Spika, fedha hizi zimegawanyika katika mafungu matatu kama ifuatavyo:-

Fungu 38 – Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

i. Bajeti ya Matumizi ya Kawaida shilingi 531,316,218,000.00

ii. Bajeti ya Matumizi ya Maendeleo shilingi 14,000,000,000.00

Fungu 39 – Jeshi la Kujenga Taifa

i. Bajeti ya Matumizi ya Kawaida shilingi 131,197,222,000.00 ii. Bajeti ya Matumizi ya Maendeleo shilingi 5,000,000,000.00

Fungu 57 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

i. Bajeti ya Matumizi ya Kawaida shilingi 15,850,052,000.00

ii. Bajeti ya Matumizi ya Maendeleo shilingi 389,186,566,000.00

HITIMISHO

62. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara yangu ina wajibu wa kusimamia matumizi bora ya rasilimali za umma, nitajitahidi kufuatilia matumizi ya fedha zitakazoidhinishwa ili tuweze kutekeleza vyema malengo muhimu yafuatayo:-

(i) Kununua zana na vifaa vya kijeshi ili Jeshi liweze kulinda mipaka ya nchi yetu kwa ufanisi.

(ii) Kujenga maghala ya kuhifadhia silaha na milipuko.

(iii) Kujenga na kukarabati nyumba za kuishi maafisa na askari

(iv) Kulipa madeni kwa kampuni zilizoliuzia zana na vifaa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

(v) Kuwapatia mafunzo vijana 5,000 kwa Mujibu wa Sheria.

63. Mheshimiwa Spika, hotuba hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara: (www.modans.go.tz). Naomba kutoa Hoja.