Tanzania emblem
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

JESHI LA KUJENGA TAIFA -JKT

Karibu

Moja ya vyombo vilivyoundwa na Serikali ya Tanganyika mara tu baada ya Taifa hili kupata uhuru ni Jeshi la Kujenga Taifa lililoasisiwa tarehe 10 Jul 1963. Jeshi la Kujenga Taifa au kwa kifupi JKT, liliundwa ili kuponya majeraha yaliyoachwa na serikali ya kikoloni miongoni mwa jamii ya watanzania ambayo ni pamoja na ubaguzi miongoni mwao katika misingi ya kidini, makabila, rangi na kipato. Chombo hiki ni muhimu katika kuelimisha na kuandaa vijana wa kitanzania kiuzalendo, kimaadili, kinidhamu na kuwafanya raia wema wanaopenda kutumikia na kulinda nchi yao.

Vikosi vya JKT ni mahali ambapo vijana hupata fursa ya kujifunza kikamilifu na kwa vitendo, maana na umuhimu wa kazi na pia kujifunza kutoa huduma kwa Taifa lao bila kutegemea kulipwa ujira wowote. Kwa hiyo, imedhihirika wazi ya kuwa wajibu wa JKT katika maendeleo ya Taifa hili ni mkubwa na muhimu sana.

Nchi mbalimbali duniani zina taasisi zinazofanana na taasisi yetu ya JKT. Kwa msingi huo nchi yetu kuwa na JKT ni jambo la kujivunia sana. JKT vilevile ni chombo cha kujenga Umoja na Utaifa kwa vijana wetu.