Tanzania emblem
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

JESHI LA KUJENGA TAIFA -JKT

Historia ya Jeshi la Kujenga Taifa

Historia ya Jeshi la Kujenga Taifa

Historia ya kuanzishwa JKT inaanzia mwaka 1958 wakati wa ziara ya viongozi wa wa Taifa nchini Ghana, ambapo Baba wa Taifa Mwl. Nyerere na Mhe. Rashid Kawawa (Simba wa Vita) walikwenda kuhudhuria sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa uhuru wa nchi hiyo.

Wakiwa nchini humo, Mhe. Kawawa alialikwa chakula cha jioni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Bi. Golda Meir.

Mhe. Kawawa alipata fursa ya kuzungumza na kiongozi huyo, ambaye alitanabaisha namna Taifa la Israel linavyowaandaa vijana wake kutumikia Taifa lao kwa moyo wa uzalendo.

‘Simba wa Vita’ alivutiwa na maelezo yaliyotolewa na Bi. Meir, namna ya utaratibu unaotumika na Taifa la Israel kuwakusanya na kuwaandaa Vijana kijeshi na baadaye kufanya majukumu mengine ya kitaifa kwa ujasiri, uvumilivu, ushirikiano na nidhamu.

Aliporejea hotelini walikofikia na Mwalimu Nyerere, Mhe. Kawawa alimwelezea juu ya mazungumzo yake na Bi. Meir, ambayo yalimvutia na kumwagiza ayafanyie kazi watakaporejea nchini.

Waliporejea, Mhe. Kawawa aliyawasilisha mawazo hayo kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU (TYL), Joseph Kizurira Nyerere, akisaidiwa na Nangwanda Lawi Sijaona. Viongozi hao waliafiki mawazo hayo na kuyapeleka katika Mkutano Mkuu wa TYL uliofanyika Tabora Agosti 25, 1958 ili kujadiliwa Zaidi na wajumbe.

Hata hivyo, mkutano wa TANU ulishindwa kuidhinisha uanzishwaji wa mafunzo hayo, kwa kuwa Tanganyika ilikuwa inatawaliwa na Uingereza chini ya ungalizi wa Umoja wa Mataifa (UNO). Baada ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961 wazo hilo liliwasilishwa kwa mara ya pili kwenye Mkutano Mkuu wa Vijana wa TANU Agosti 25, 1962 mjini Tabora.

Mkutano huo uliazimia kutekeleza wazo la kuanzishwa rasmi kwa taasisi ya kuandaa Vijana kuwajengea uzalendo na umoja wa kitaifa. Wajumbe wa kikao hicho walikuwa Joseph Nyerere (Mbunge na Katibu Mkuu TYL), Isack Malecela (Katibu Mkuu wa Mambo ya Fedha TYL), Moses Nnauye, H.S.J Zingaro (Katibu mkuu Mtendaji TYL) na Meja Yaffer Ben Amots wa Israel (mshauri mtaalamu wa mpango huo).

Baada ya mkutano huo, mapendekezo ya kuanzishwa chombo rasmi cha kitaifa cha kuandaa Vijana kuwa Wazalendo, yaliwasilishwa serikalini na kuidhinishwa na Baraza la Mawazili Aprili 1963.

Serikali iliridhia chombo hicho kiitwe Jeshi la Kujenga Taifa chini ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Wizara hiyo iliongozwa na Waziri Nangwanda Sijaona (Mwenyekiti TYL), Joseph Nyerere (Naibu Waziri na Katibu TYL) na Mzee Harubu Saidi (Katibu Mkuu wa Wizara).                                                                 

Julai 10, 1963 ilianzishwa rasmi bila kutungwa sharia na Bunge la Tanganyika.

Sheria ya Kuanzishwa kwa JKT

JKT ilianzishwa kwa Sheria Namba 16 (National Service Act, 1964) iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 kifungu 3(1). Sheria hii ilipitishwa kuwataka vijana kujitolea kwa hiari kujiunga na JKT ili kulitumikia Taifa. Vijana hao walitakiwa kuwa angalau wawe wamehitimu elimu ya msingi, wanachama wa TYL, wasiwe wameoa au kuolewa na wawe tayari kujitolea kutumikia Taifa kwa muda wa miaka miwili. Baada ya kupitishwa sheria hiyo, Novemba 1964 kundi la kwanza liliripoti Mgulani JKT na kuitwa Operesheni Maendeleo, likiwa na vijana 486.

Kurejeshwa kwa Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria

Kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria ilikuwa ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha juu katika awamu ya nne ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Serikali ya awamu ya nne imerudisha mafunzo ya JKT kwa sababu ya nia njema ya kuendelea kujenga uzalendo kwa vijana wa Tanzania. Itakumbukwa kwamba kutokana na hali ngumu ya kiuchumi Serikali ilishindwa kumudu kuendesha mafunzo ya JKT kwa mujibu. Mnamo Juni 15, 1994 mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria yalisitishwa kwa muda.

Jeshi la Kujenga Taifa limefanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia katika Jeshi hilo. Hapa ni mahali ambapo vijana wa itikadi zote, rangi zote, makabila yote, dini zote hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa familia moja.

Hakuna chombo chochote cha malezi ya vijana kilichoizidi JKT katika kazi hiyo, pengine hata ile tabia ya Watanzania wengi kutoulizana makabila yao inatokana na uwepo wa JKT. Vijana wazalendo wa Tanzania wanaopitia JKT huwa wanakutana na vijana mbalimbali kutoka kila kona ya nchi yetu, ndiyo maana hawana muda hata wa kuulizana makabila kwa vile wote hujiona ni wamoja.

Aidha, athari za kusimamishwa kwa mafunzo ya JKT kuliwagusa wengi na ndiyo maana Serikali ya awamu ya nne imerejesha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria. Hatimaye tarehe 26 Machi 2013 mafunzo ya JKT yalianza ikiwa ni pamoja na kutimiza ahadi ya serikali ya kufufua upya mafunzo hayo katika kambi ya Ruvu.

Kama ilivyokuwa mwaka 1964 JKT ilipoanza na mwaka 1968 baada ya mafunzo ya mujibu wa Sheria kuanzishwa viongozi wa kitaifa waliongoza katika kushiriki mafunzo hayo. Mafunzo hayo ya JKT yalianza na kulikuwa na idadi ya wabunge 22 ambao walishiriki na kumaliza mafunzo ya uongozi. Wabunge hao walitawanywa katika kambi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya muda wa miezi miwili waliyoomba wenyewe kwa ajili ya kupata mafunzo ambayo wanaamini yatawajengea uzalendo zaidi kwa taifa lao.

Viongozi wa Kitaifa Waliofanya Mafunzo ya JKT

Kuanzia mwaka 1968, Viongozi wa Kitaifa walihamasika kufanya mafunzo ya JKT. Miongoni mwao ni;

  • Mwalimu Nyerere – Operesheni Mwenge JKT Mafinga mwaka 1968.
  • Mhe. Aboud Jumbe Mwinyi (Makamu wa Kwanza wa Rais)
  • Mhe. Kawawa (Waziri Mkuu na Makamu wa Pili Rais)
  • Mhe. Adam Sapi Mkwawa (Spika wa Bunge)
  • Mhe. Edward Moringe Sokoine (Waziri wa Ulinzi)
  • Mhe. Job Lusinde (Waziri wa Mawasiliano)
  • Mh.  Abdulrahman Mohammed Babu (Waziri wa Mambo ya Nje) na wengineo ambao wote walipata mafunzo JKT Ruvu Operesheni Kazi ‘B’ mwaka 1968.
  • Mhe. Benjamini Mkapa (Mhariri Mtendaji a Gazeti la Uhuru baadaye Rais wa Tanzania) alifanya mafunzo JKT Ruvu, Operesheni Tekeleza mwaka 1971.
  • Mhe. Benard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mstaafu) alifanya mafunzo JKT Oljoro, Operesheni Muungano (JW & JKT) mwaka 1975/76.

Aidha, Vijana wengi wa kitanzania walipata fursa ya kutumikia Taifa kupitia JKT na baadaye kuwa viongozi. Miongoni mwao ni:

  •   Mhe. Othman Chande (Jaji Mkuu Mstaafu) Operesheni Utii mwaka 1967.
  • Mhe. Zakhia Meghji (Waziri wa Fedha Mstaafu) Operesheni Utamaduni mwaka 1969.
  • Mhe. Fredrick Sumaye (Waziri Mkuu Mstaafu) Operesheni Mwangaza mwaka 1970.
  • Mhe. Edward Lowassa (Waziri Mkuu Mstaafu) Operesheni Mikoa JKT Ruvu mwaka 1970.
  • Mhe. Mizengo Pinda (Waziri Mkuu Mstaafu) Operesheni Mikoa JKT Ruvu mwaka 1970.
  • Mhe. Dkt.Jakaya Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne) Operesheni Tumaini, JKT Ruvu, mwaka 1972.
  • Jenerali Salvatory Venance Mabeyo (Mkuu wa Majeshi Mstaafu) Operesheni Usafi, JKT Mafinga, mwaka 1978.
  • Meja Jenerali Michael Isamuhyo (baadaye alikuwa Mkuu wa JKT) Operesheni Mazoezi JKT Ruvu, mwaka 1978.
  • Mhe. Dkt. John Magufuli (Rais wa awamu ya Tano) Operesheni Mshikimano JKT Makutupora mwaka 1984.
  • Mhe. Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu) Operesheni Kambarage JKT Mlale mwaka 1990/91.
  • Meja Jenerali Rajabu Mabele (Mkuu wa JKT) Operesheni Kambarage JKT Ruvu mwaka 1990/91.
  • Jenerali Jacob Mkunda (Mkuu wa Majeshi) Operesheni Vyama Vingi, JKT Ruvu mwaka 1992.

 

WABUNGE WALIOFANYA MAFUNZO YA JKT.

Wafuatao walifanikiwa kupitia Mafunzo ya JKT baada ya kurejeshwa.

Kambi ya JKT Ruvu wabunge tisa walihitimu akiwemo

1. Mhe. Mendrad Lutengano Kigola (MB).                                    (Kambi RUVU)

2. Mhe. David Ernest Silinde (MB).                                                 (Kambi RUVU)

3. Mhe. Easter Amos Bulaya (MB).                                                 (Kambi RUVU)

4. Mhe. Murtaza Mangungu (MB).                                                   (Kambi RUVU)

5. Mhe. Yusuph Haji Khamis (MB).                                                 (Kambi RUVU)

6. Mhe. Neema Mgaya Hamis (MB).                                                (Kambi RUVU)

7. Mhe. Halima James Mdee (MB).                                                 (Kambi RUVU)

8. Mhe. Livingstone John Lusinde (MB).                                       (Kambi RUVU)

9. Mhe. Said Mohamed Mtanda (MB).                                            (Kambi RUVU)

10. Mhe Sabreena Sungura (MB).                                                   (Kambi BUROMBORA)

11. Mhe Seleman Said Jafo (MB).                                                   (Kambi BUROMBORA)

12. Mhe Mariam Kasembe (MB).                                                     (Kambi BUROMBORA)

13. Mhe Mariam Salum Msabaha (MB).                                         (Kambi BUROMBORA)

14. Mhe Yahaya Kasim Issa (MB).                                                  (Kambi BUROMBORA)

15. Mhe Zitto Z. Kabwe (MB).                                                         (Kambi MGAMBO)

16. Mhe Raya Khamis (MB).                                                           (Kambi MGAMBO)

17. Mhe Dr. Anthony G. Mbassa (MB).                                          (Kambi MGAMBO)           

18. Mhe Idd Azzan (MB).                                                                 (Kambi MGAMBO)

19. Mhe Abdallah Hajji Alli (MB).                                                    (Kambi MGAMBO)

20. Mhe Meshack Mfukwa (MB).                                                    (Kambi MSANGE)

21. Mhe Rita Kabati (MB).                                                               (Kambi MSANGE)

22. Mhe Mwigulu Lameck Nchemba (MB).                                    (Kambi MSANGE)

 WAKUU WA JKT

Wafuatao ni wakuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963.

1.         ASP David Nkulila                                                    -           (1963-1967)

2.         ASP Robert Kaswende                                             -           (1967-1970)

3.         ASP Laurence Gama                                                -           (1970-1973)

4.         Meja Jenerali Nelson Mkisi                                      -           (1973-1989)

5.         Meja Jenerali Makame Rashidi                               -           (1989-2001)

6.         Meja Jenerali Davis Mwamunyange                       -           (2001-2006)

7.         Meja Jenerali Abdulrahman Shimbo                      -           (2006-2007)

8.         Meja Jenerali Martin Madata                                  -           (2007-2008)

9.         Meja Jenerali Samwel Kitundu                               -           (2008-2012)

10.       Luteni Jenerali Samweli Ndomba                           -           (2012-2012)

11.       Meja Jenerali Raphael Muhuga                              -           (2012-2016)

12.       Meja Jenerali Michael Isamuhyo                             -           (2016-2019)

13.       Meja Jenerali Martin Busungu                                -           (2018-2019)

14.       Brigedia Jenerali Charles Mbuge                            -           (2019-2021) 

15.       Meja Jenerali Rajabu Mabele                                  -           (2021-Hadi sasa)