Tanzania emblem
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

JESHI LA KUJENGA TAIFA -JKT

JKT Lang'ara Maonesho Sabasaba

15 Jul, 2022
JKT  Lang'ara Maonesho Sabasaba

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali ( SUMAJKT) Kanali Petro Ngata amesema siri ya ushindi wa tuzo walizopata katika kilele cha Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) mwaka huu 2022  ni nidhamu, Weledi na kuwatumia Wataalamu wazuri waliopo ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT). 

Kanali Ngata amesema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya JKT kutangazwa washindi wa tuzo tatu zilizotolewa na TANTRADE, ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alikuwa Mgeni Rasmi.

Akimwakilisha Mkuu wa JKT na Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT Meja Jenerali Rajabu Mabele, Kanali Ngata amesema SUMAJKT kupitia Kampuni Tanzu, Miradi na Kanda za Ujenzi limeendelea kuzalisha bidhaa bora, kutoa huduma na kufanya Biashara kwa weredi sambamba na kutekeleza miradi yake kwa wakati, ubora na weredi. hivyo kupelekea kupata ushindi.

JKT kupitia SUMAJKT limetangazwa ushindi wa kwanza katika kipengele cha Uzalishaji wa Bidhaa Bora nchini, Ushindi wa kwanza katika Kilimo Mifugo na Uvuvi na mshindi wa pili katika kipengele cha Utengenezaji wa  Samani bora hapa nchini.

Kanali Ngata amesema JKT limeongeza uzoefu wa kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa kwenye mataifa mengine ambapo mwezi Mei mwaka huu, lilishiriki kwenye maonesho kama hayo nchini Comoro na kupata ushindi na kufanya biashara nchini humo hatua inayozidi kuwaongezea uzoefu wa maonesho kama hayo.

Maonesho hayo ya Kibiashara Kimataifa yanayofanyika kila mwaka ifikapo Julai, ambapo msimu huu yameonesha mafanikio makubwa chini ya Kauli Mbiu; "Tanzania: ni Mahala sahihi pa Biashara na Uwekezaji"